Huawei yatoa tuzo kwa washindi wa hackathon yenye mahitaji maalum nchini Kenya
Kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya China ya Huawei imetoa zawadi mbalimbali siku ya Jumanne, yakiwemo makombe, vyeti na vifaa vya kielektroniki, kwa washindi wa hackathon wenye mahitaji maalum, ambayo ilizinduliwa nchini Kenya mwezi Machi.
Washindi hao wakiwemo wanafunzi wa chuo cha Huawei ICT, walitambuliwa kwa kutoa suluhu bora za kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu. Maafisa wakuu wa serikali na watendaji wa Huawei walihudhuria hafla hiyo ya utoaji tuzo, iliyofanyika kando ya mikutano ya kila mwaka ya Benki ya Maendeleo ya Afrika jijini Nairobi.
Ofisa Uhusiano wa Umma katika kampuni ya Huawei Kenya, Winnie Chepkonga, amesema mashindano ya hackathon ya Akili Mnemba (AI) ni muhimu kwa ajili ya kuhimiza wanafunzi kuvumbua kwa manufaa ya wale walio na ulemavu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Maalum ya Kenya, Norman Kiogora, amesema kupitia ushirikiano na Huawei, taasisi hiyo itaweza kuimarisha upatikanaji wa teknolojia zinazowezesha watu wanaoishi na ulemavu.
Kiogora amesisitiza kuwa kwa kutumia AI, watu wenye mahitaji maalum wanaweza kupata ujuzi wa maisha, kuunganishwa katika uchumi wa kawaida, na kuwa na ufahamu zaidi wa mazingira yao.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma