Rais Biden aidhinisha msaada zaidi wa kijeshi wakati Rais wa Ukraine Zelensky akitembelea Washington
Rais wa Marekani Joe Biden (Kulia) akiwa katika picha na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Desemba 21, 2022. Rais wa Marekani Joe Biden Jumatano amemuahidi Rais wa Ukraine aliyezuru Washington Volodymyr Zelensky kutoa msaada wa kijeshi, akitaja msaada wa makombora ya kufyatuka kutoka ardhini hadi angani ambao umeidhinishwa hivi punde kwa Ukraine katika usaidizi mpya wa kiulinzi wenye thamani ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.85. (Xinhua/Liu Jie)
WASHINGTON, - Rais wa Marekani Joe Biden Jumatano amemuahidi Rais wa Ukraine aliyezuru Washington Volodymyr Zelensky kutoa msaada wa kijeshi, huku akitaja msaada wa makombora ya kufyatuka kutoka ardhini hadi angani ambao umeidhinishwa hivi punde kwa Ukraine katika usaidizi mpya wa kiulinzi wenye thamani ya jumla ya dola za kimarekani bilioni 1.85.
Kwa mujibu wa orodha kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, shehena ya silaha zilizoidhinishwa na Biden, pia inajumuisha "silaha za angani za kulenga kwa usahihi," ambazo haikuelezwa kwa undani kuhusu aina na idadi. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, huenda zikawa zile zinazoitwa "Mashambulizi ya Pamoja ya Moja kwa Moja," ambazo hubadilisha mabomu "bubu" yasiyozuiliwa kuwa mabomu "shambulizi" kwa kuongeza mapezi na mfumo wa mwongozo wa kulenga kwa usahihi.
Alipowasili Marekani Jumatano kwa ajili ya ziara, Zelensky alimwambia Biden kwamba alitaka "kuja mapema" lakini hakuweza kwa sababu ya hali ngumu ya Ukraine ambayo sasa imedhibitiwa.
Ingawa Zelensky alimsifu Biden, hakumung’unya maneno lilipokuja suala la silaha za betri ya Patriot -- mfumo wa silaha wa hali ya juu zaidi ambao Marekani imetoa na kitu ambacho Zelensky amekuwa akiomba kwa muda mrefu. Alimwambia mwenzake kwamba silaha hiyo moja tu haitoshi kwa Ukraine.
"Tungependa kupata silaha za Patriots zaidi," Zelensky alisema na kufuatiwa na kicheko kutoka kwa Biden, ambaye alisimama karibu naye kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mkutano wao wa pande mbili.
Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari Biden amesisitiza kuwa Marekani imejitolea kuhakikisha kuwa Ukraine inaendelea kuwa na uwezo wa kujilinda bila kujali "ni muda gani itachukua".
Zelensky aliwaambia waandishi wa habari kwamba amependekeza kwa Biden wazo la "mpango wa kimataifa kwa ajili ya mkutano wa kilele wa amani" na kutoa "hatua mahususi ambazo Marekani inaweza kufanya ili kutusaidia kutekeleza." Hakufafanua zaidi.
Rais wa Ukraine alisema baadaye alipokuwa akitoa hotuba katika kikao cha pamoja cha Mabunge ya Marekani ya Baraza la Chini na Juu kwamba mpango wa amani aliopendekeza una "vipengele 10," kwamba mkutano huo wa kilele "unaweza kufanyika," na kwamba "Rais Biden aliunga mkono mpango wetu wa amani leo."
Hata hivyo, John Kirby, mratibu wa Baraza la Taifa la Usalama la Marekani kwa mawasiliano ya kimkakati, ameliambia Shirika la Habari la CNN kwamba "ni wazi Zelensky anataka kutafuta amani ya haki kuendana na kile anatamani".
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma