Jumuiya ya Wachina yatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 100 wa Zimbabwe
HARARE - Wanafunzi mia moja kutoka shule kumi za msingi zinazosimamiwa na manispaa katika Mji Mkuu wa Zaimbawe, Harare, watafaidika na ufadhili wa ada za masomo chini ya Ufadhili wa Masomo wa Urafiki kati ya China na Zimbabwe.
Mpango huo wa ufadhili wa masomo ambao umezinduliwa rasmi Jumatano wiki hii mjini Harare, unawezeshwa na Kituo cha Mabadilishano na Utafiti wa Kiuchumi na Kitamaduni cha China na Afrika (CAECERC) kwa uungaji mkono wa makampuni kutoka China yaliyowekeza nchini Zimbabwe.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, ambapo baadhi ya wanufaika walikabidhiwa fedha za ufadhili, mwakilishi wa wakuu wa shule za msingi za halmashauri mjini Harare, Stellah Gunje, ametoa shukrani kwa Wachina hao kwa hatua hiyo nzuri.
"Wanafunzi wasio na uwezo au wanafunzi katika shule zilizochaguliwa za halmashauri wana kitu cha kuwafanya watabasamu. Ni ndoto iliyotimia kwa wanafunzi hao," amesema.
Kaimu Meya wa Harare Stewart Mutizwa amesema mpango huo unaendana na azma ya halmashauri ya jiji kutoa elimu kwa gharama nafuu kwa wanafunzi wote.
“Hakuna shaka kuwa msaada huu utawapa motisha na kuwatia moyo wanafunzi wengi kuongeza bidii ili wawe sehemu ya mpango huu,” amesema.
Mpango huo pia utapanuliwa ili kunufaisha shule nyingine za halmashauri na serikali kote nchini.
Mbali na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa shule za msingi, Ufadhili wa Masomo wa Urafiki kati ya China na Zimbabwe tayari unatoa msaada kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Hadi sasa wanafunzi thelathini kutoka vyuo vikuu vitatu vya serikali nchini Zimbabwe wamenufaika na mpango wa ufadhili wa masomo.
Steve Zhao, Mkurugenzi wa CAECERC, amesema mpango huo ni sehemu ya uwajibikaji wa kijamii wa makampuni kutoka China, akidai mpango huo umetekelezwa baada ya kubaini kuwa changamoto za kiuchumi zinazosababishwa na janga la UVIKO-19 zimesababisha wazazi wengi kutoka katika mazingira duni kushindwa kupata fedha za kuwapeleka watoto wao shule.
China imekuwa ikisaidia sekta ya elimu nchini Zimbabwe tangu nchi hiyo ilipopata uhuru Mwaka 1980. Imetoa ufadhili wa masomo kwa zaidi ya wanafunzi 100 wa Zimbabwe kila mwaka kupitia ufadhili wa masomo wa Serikali ya China, ufadhili wa masomo wa Taasisi ya Confucius, ufadhili wa masomo wa serikali za mikoa mbalimbali ya China pamoja na ufadhili wa masomo unaofadhiliwa na makampuni ya kibiashara ya China yaliyowekeza nchini Zimbabwe.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma